Mwanzo 2
MLANGO WA 2
Basi mbingu na nchi
zikamalizika, na jeshi lake lote.
2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote
aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote
aliyoifanya.
3 Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa
sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba
na kuifanya.
4 Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi
zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi
5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya
kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala
hapana mtu wa kuilima ardhi;
6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya
uso wote wa ardhi.
7 Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi,
akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.
8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa
mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.
9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti
unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya
bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
10 Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani
maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne.
11 Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka
nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu;
12 na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna
bedola, na vito shoham.
13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka
nchi yote ya Kushi.
14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio
unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.
15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika
bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema,
Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na
mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
18 Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke
yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.
19 Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi
kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone
atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake.
20 Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa
kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa
kumsaidia Adamu aliyefanana naye.
21 Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito,
naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,
22 na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana
Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.
23 Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika
mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana
ametwaliwa katika mwanamume.
24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama
yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.
25 Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe,
wala hawakuona haya.
Comments
Post a Comment